Thursday, November 6, 2025

KULITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI (PART 8)

*KULITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI*
_*Rightly Dividing The Word of Truth*_ (2Timothy 2:15b)

*SEHEMU YA NANE*

*A.) MWAMINI AMEITWA KUWA HURU*

Mwandishi: *Mwl Proo*


Maandiko: Wagalatia 5:13, Yohana 8:32, 36

Salaam wapendwa katika Bwana na Mwokozi, Yesu Kristo! Nawakaribisha kuendelea kujifunza kweli ya neno la Mungu. Kila mhudumu wa kweli wa injili, atafurahishwa daima na kazi ya kuwaelekeza waamini katika kweli. Wapenda sarakasi, hata wakiijua kweli mioyoni mwao, hawataisema, kwani ni wanufaika wa ujinga wa waamini. Wiki chache zilizopita nimemsikia mhubiri wa kilokole anafundisha somo, "Jinsi waamini wanavyologwa kieneo". Katika ufafanuzi wake alisema unaweza kuwa umeokoka vizuri, lakini kibiashara ukiwa mkoa fulani haufanikiwi, ukiwa mkoa mwingine unafanikiwa, kwa sababu umelogwa kieneo. Vyovyote tu vile atakavyoipamba...!!! Vipi na yeye mhubiri amelogwa kieneo? 😂. Kama kuna jambo alilifanya likasaidia yeye asilogwe kieneo, basi afundishe mara moja jambo hilo, ili hawa waumini wake wasilogwe tena kama yeye ambavyo halogwi, kisha aachane na hizo jumbe.... Lakini jumbe na mafundisho haya, mara nyingi huambatana na kutoa fedha na mali kama namna ya kusindikizia maombi ili kuwaepusha na kulogwa kieneo.... The same the same message, itarudiwa tena ikiwa na sura tofauti ikionesha kwa nini pesa zinapotea, kwa nini unapoteza kibali, kwa nini watoto wanafeli.... (jumbe fukunyuzi, za kutafuta wapi mwamini atapumbazwa, asahaulishwe msalaba wa Kristo). Wenzetu mnahubiri Ukristo gani? Mmeyapata hayo kwa Yesu yupi? Mnachofundisha na kuhubiri mnakutana nacho kwenye nyaraka 21 za mitume popote? Au ndio mafunuo binafsi?

Ukristo, mikononi mwa watu wasio imara kwenye mafundisho, kwenye kupuuza kabisa kanuni za kutafsiri maandiko, umekuja kuwa kama *CULT* kama  *VOODOOISM*, yaani ni ki-movement fulani hivi cha ubabaishaji... mahali tu unapokuja kuoneshwa wewe ni mfungwa, tegemezi, upo katika hatari daima, mnusurika wa daima, mlaaniwa ambaye laana zitaendelea kuondolewa taratibu, kwa kadri kiongozi wako wa dini atakavyoendelea kufunuliwa..!. Huwa nasikiliza mafundisho ya Ukristo kwa TV, mpaka nahoji sasa kama Ukristo ni zigo zito hivi... mnahubiri nini sasa? Mnawakaribisha watu waje wafanye nini? Mbona ni kama wao wapagani wako huru kuliko ninyi huku? Mnawaalika waje walogwe pamoja nanyi?


*B. KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU*

Efeso 4:13-16, Kolosai 1:26-28
Waamini wanaweza wakakoseshwa shabaha, kama baada ya kuamini watafundishwa elimu zingine.. huku wakiamini kwamba wamezaliwa na Mungu ili wawe matajiri wa kumiliki mali mengi, kwamba sasa wao watakuwa wajasiriamali nambari moja, watakuwa wawekezaji kwenye uchumi namba moja... Na hapa ndipo maandiko kama 2Korintho 8:9, kwamba Yesu alifanyika masikini ili wao wawe matajiri, mara Mwanzo 12 & 15, baraka za Ibrahim bla bla, kwa bahati mbaya sana kule kupuuzia kanuni za kutafsiri maandiko ndiko kumefanya maandiko hayo hapo juu yahusishwe na utajiri wa kumiliki mali (Kanuni ikizingatiwa tu juu ya hayo maandiko, kinachotajwa ni kuhesabiwa haki bure kwa njia ya imani, kuokolewa kwa kumwamini Yesu tu). Mwamini, anapaswa amfahamu sana, sana, sana, Mwana wa Mungu. Siri zote, utimilifu wote wa Mungu, unakaa katika Yeye, Yesu. Unampofunzwa sana kuhusu Mwana wa Mungu, ili umfahamu sana, ndipo sasa na wewe utajifahamu sana. Utakuwa mtu mkamilifu, aliyekuwa kiroho, mwenye kimo cha cheo, kama Kristo, kwa kuwa umemfahamu sana Mwana wa Mungu... Utakuwa huru, mbali na vifungo, mbali na kuonewa, mbali na giza lote kwa sababu umemfahamu sana Yesu. Struggles za kupambana na mwili, na matendo yake, maisha ya kujazwa hofu, kutembea tena kama mtumwa baada ya kuzaliwa na Mungu, ni product ya mafundisho...  Hakuna mwamini aliyejifunza kwa ufasaha kuhusu Yesu, atakaa kwenye kiti 🪑 afundishwe tena namna alivyologwa kieneo... Afundishwe tena namna kitovu chake kilichawiwa na mabibi, namna alivyoibiwa nyota yake, namna wachawi wanavyoyafunga maisha yake sijui aje aje... Kusikiliza tu fundisho kama hilo ni kuyatia maarifa giza... Giza haliiwezi nuru (Yohana 1:4-5), hakuna siku balbu ya umeme yenye 100 watts, itawashwa chumbani  kisha giza ligome, kwamba taa waka, na mimi giza nabaki kama kawaida... Yesu ni nuru, amewafanya waamini nao kuwa nuru (Mathayo 5:13-14), mnakuwaje nuru mkiwa mnafundishwa vitu vya kuwatia utumwa? Mtafunguaje watu wa mataifa iwapo ninyi daima ni manusura wa hivyo vifungo, mnaoponea chupu-chupu kwa kudra za huyo mhubiri wa kwenu? Yaani kwamba asingekutabiria tu juu ya shida zako, kwishaaaaaaa! ilikuwa nawe usombwe na maji... Akakutabiria kwamba anaona umelogwa, anaona mikwamo, anaona majanga, mambo hayasogei, anaona umepoteza kibali... Haya yalikukuta yote ukiwa wapi mwenzetu??? Au labda ndio umekuja kuisikia injili? Yaani umezaliwa na Mungu, unakaliwa na Roho wake milele, Mungu amechagua kwa hiari yake afanye makao ndani yako milele, una ushirika naye milele, umeketishwa na Yesu juu sana, lakini pamoja na hayo hapa kati umeibiwa nyota, umepoteza kibali, umelogwa kieneo, umefungwa usiolewe na kuoa... Kama hili ni kweli, basi Ukristu unakuwa ni matakataka kabisa... Kama ukiwa na Mungu ndani yako, una ushirika naye, umefanyika mfalme na kuhani, lakini kuna mwizi mchawi, bado anakuibia kibali na nyota, ni nini sasa kitazuia asikuibie tena? Aliwezaje mwanzo, atashindwaje baadaye.... Haya yanashamiri kwa sababu kuna wanufaika wa ujinga wa waamini, kuna  mtu anajijenga kiuchumi in the expense of believers' ignorance.. Yeye peke yake haibiwi nyota, hafungwi, halaaniki, halogwi (mkingiwa wa majanga yote) lakini anaowaongoza kiroho pekee wako _prone and vulnerable to all sorts of disasters_ (HUU NI UTAPELI TU WA KAWAIDA). Imagine mhubiri kwenye TV anaelekeza watu, kuwa kinachofanya wanapitia matatizo ya kwenye ndoa yao, ni kwa sababu ile mahari iliyolipwa kabla waowane, hawakuitolea fungu la kumi... 😥😥😥 !!!  Huyu ndiye mwamini wa nyakati hizi na chakula anacholishwa kiroho. Mimi pia kuna nabii alipoona nakawia kuoa, aliniambia, akiwa katika maombi, Mungu alimfunulia kuwa kuna sadaka maalumu ilitolewa kwenye madhabahu ya kuzimu, kuzuia ndoa yangu, kuhakikisha kwamba sioi... Hiyo siku aliyoniambia hivyo kwa njia ya WhatsApp, niliweka tu emoji za kulia (😭😭😭😭😭😭😭) wala sikuandika kitu kingine, maana nilikuwa na safari siku ya kesho yake kwenda kulipa mahari... Na nikaoa miezi mitatu baadaye bila kuhangaika na kafara maalumu kwenye madhabahu ya kuzimu... Fikira kama nisingejenga msingi imara kwenye kweli ya Kristo, na namna ambavyo ningeanza kukimbizana na kafara ya kuzimu inayozuia ndoa...!



*BIBLIA INASOMWA, NA INAFUNDISHWA KIFUNDISHO*

Bila kusahau msisitizo wa kanuni za kutafsiri maandiko (Hermeneutics), zilizodadavuliwa kwa upana sehemu ya I, II, & III, ya mfululizo huu, jambo jingine la msingi la kujua ni kwamba Biblia inasomwa na inafundishwa kifundisho. 
Watu wanaotafuta uvumbuzi wao kwenye maandiko (Eisegesis), wanaweza kusoma Ufunuo wa Yohana 8:13 (Kuhusu tai 🦅 arukaye), na wakahitimisha huyu tai anawakalisha taifa la Marekani, kitu ambacho hata mtume Yohana aliyeandika hakuwahi kuwaza. Ni uchaguzi wa kutoisoma Biblia, na kuifundisha kifundisho...

KUISOMA BIBLIA KIFUNDISHO...  ni kuiangalia yote kwa pamoja (synoptically), kutazama kiini cha ujumbe, ushabihisho kimuktadha, na ya KUIFUNDISHA KIFUNDISHO ni kujiuliza, hiki nilichosoma, kilifundishwa hivyo kwa waamini?. Hapa utakuwa salama!
Wiki chache zilizopita nimeona tangazo la ibada maalumu, ya kuwatenganisha waumini walokole, na malkia wa mbinguni, pamoja na kuondoa laana za kwenye majina yao zilizowaingia kupitia vyakula. Nilistuka kuona tangazo kubwa limerembwa vizuri kwa rangi za kuvitia, na wahubiri kama 7, lakini maombi maalum ni kuwatenga kwa maombezi, washirika na malkia wa mbinguni.... Hawa watu walisoma vifungu vitano katika Yeremia, ambaye yeye peke yake alimtaja mungu mke wa kipagani (isthar) kwa kificho, kama malkia wa mbinguni .. ambapo wana wa Israel waliwahi kumwabudu kwa kuCopy utamaduni wa kipagani na kumfanyia ibada kwa kukanda unga, kutengeneza kaki (keki) na kumwaga vinywaji. Swali linakuja; hawa waamini wa injili ya Yesu Kristo, waliozaliwa na Mungu, na kukaliwa na Roho wa milele... Waliunganishwa lini na Isthari au Ashtorethi (pagan goddesses), kiasi cha kuhitaji maombi ya kuwatenganisha nao? Mlipata wapi giza la kuwapaka waamini wanaoonekana kama mianga, hawa ambao ni nuru ya ulimwengu? Mshirika wa Kikristo, ambaye anakuja kanisani akiwa ameelekezwa tayari ameunganishwa na malkia wa mbinguni (labda niite falme za giza, majini/mapepo), huyu atashindwaje kupata uvamizi wa roho za giza? Maana fundisho hilo tayari limeunda fikra, badala atembee njiani akijijua kuwa ameketishwa juu sana, pamoja na Kristo, juu sana zaidi ya kila jina, zaidi ya kila ufalme, usultani, ubaba, juu sana kuliko majeshi ya pepo, juu sana kuliko wakuu wa giza... Anaenda kanisani na kasadaka
ka elfu 5 Tshs ziwezeshe mchakato wa kumtenganisha na malkia wa mbinguni...  Wapi mambo haya? Je! mitume wa Kristo walisahau kulitenga kanisa la kwanza na huyo mungu mke wa kipagani? Je! waliposoma Yeremia 7:18 walitoka na fundisho kama lako?
Last week, nimekutana tena na kitu cha ajabu kwenye TV... (Mhubiri wa Assemblies Of God toka Dar), amesoma Hesabu 23, kisa cha zile sadaka ambazo mchawi na mnajimu Balaamu bin Beori alimwelekeza Balaki bin Sipori kuzitoa ili yeye akakutane na Bwana, kisha akazipa jina kuwa ni *"sadaka za udhamini"*.. Baada ya hapo akasisitiza sana, kuwa ni lazima kutoa sadaka za udhamini, mtu hatatoboa asipotoa hizo sadaka za udhamini... Wapi mambo haya? Kusoma na kufundisha maandiko kifundisho ni pamoja na kuhoji, Je! ndivyo walivyofundishwa waamini? Je! inashabihiana na ujumbe wa Mungu kwa waamini katika Kristo? Fundisho kwa waamini linatazamwa synoptically throughout the Bible... ndio maana ni muhimu kujua, Biblia iko na kiini cha ujumbe (the central message).  Inaweza kujadili ujenzi wa ukuta wa mji, wala haina maana sasa Biblia ni kitabu cha architectural studies, inaweza kuwa na visa vya kusimamia biashara, wala haitakuwa na maana sasa Biblia tayari ni kitabu cha business management... Kabla hujaokoteza maandiko popote, ukihisi unapata ufunuo, ujiulize kama usomaji na ufundishaji wako upo kifundisho? Je! hauwatii waamini katika utumwa? Je! hauibatili neema ya Mungu? Je! hauufanyi msalaba wa Kristo kuwa bure na usio na maana? Je! haujiinui wewe kuwa mwokozi msaidizi, kana kwamba Yesu hakupatia sana suala la wokovu, ila unayo namna nyingine ya kuvumbua vifungu vya kupachika vifungo kwa waamini?


*MWAMINI UMEITWA UWE HURU, MFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU UTEMBEE KATIKA UHURU KAMILI*


Tukutane kwenye sehemu ya 9 ya mfululizo wetu.
Mmebarikiwa, Shalom Aleichem! 👋

No comments:

Post a Comment