*ROHO YA CHOYO*
Mwl Proo
+255762879363
Amani iwe kwenu!
Andiko la msingi
*“Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.”*
— Luka 12:15
Tabia nyingi zinazojidhihirisha kwa matendo, ni matokeo ya ushawishi (influence) ya roho/spirits. Hapa sasa hata mwamini asipokuwa na nuru ya kutosha inayotokana na maarifa ya neno la Kristo, naye anaweza akashawishiwa na roho nyingine isiyo ya Kristo. Mwamini tangu anapoifahamu ile kweli (hawezi tena kumilikiwa na pepo i.e., _demon-possessed_), lakini suala la kushawishiwa (being influenced) na roho isiyo ya Kristo bado litawezekana tu, itategemea ni kwa kiwango kipi nafsi yake imejengwa (1Korintho 14:4) na kiwango cha ufahamu na maarifa ya kiroho anayotembea nayo katika kumjua Kristo.
(Visit Mwl Proo Tv on YouTube for more sermons)
Napenda kuutumia mfano wa Petro, yeye kama mmoja wa watu waliokuwa karibu sana na Yesu, tunaona katika (Mathayo 16:16-17) anaongozwa/shawishiwa na Roho wa Mungu kumtambua Yesu. Lakini mtu huyo huyo mbele kidogo katika sura hiyo (Mathayo 16:22-23) anashawishiwa na roho isiyo ya Mungu kufanya jambo lingine, ambapo Yesu anamkemea akijua nyuma ya mawazo ya Petro kuna ushawishi wa shetani. Kumbuka pia kile kilichotokea kwa Yohana na Yakobo (Luka 9:54-55), wao waliona wako sahihi kabisa kushusha moto uwaue watu waliokataa kuwakirimu. Yesu alijua wazo hilo halijatokana na ushawishi wa Roho wa Mungu, ila ni roho nyingine ya uharibifu imewatia ushawishi. Huenda ukasema, hawa walionesha tabia hizi kwa kuwa ilikuwa ni kabla ya mauti ya msalaba, hebu fikiria tabia ya kinafiki aliyoionesha Petro (na akina Barnaba) akiwa amejaa Roho tayari yaani amezaliwa upya na amekuwa mtume mwenye uzoefu mwingi (soma Wagalatia 2:11-17). Hii inatuambia hata mwamini anaweza kushawishiwa na roho nyingine kutenda matendo fulani yasiyopatana na tabia za mtoto wa Mungu.
*MOYO WA SOMO*
Kwa kutambua hayo yaliyo katika utangulizi, hiki anachokisema Yesu kwenye Luka 12:15, kujilinda na choyo ni zaidi ya tabia tu, bali tabia inayoshawishiwa na roho (roho ya choyo) ambayo hata mtoto wa Mungu asipoangalia anaweza kujiingiza katika mtego wa hii roho. Somo hili nimeliandika leo 11/8/2022 lakini nililipata mwaka 2017. Na lilinijia kama wazo baada ya kijana fulani ambaye nilikuwa naye kwenye kundi la VIJANA NA MAISHA la WhatsApp, kunifuata inbox kunisihi akisema, *"Nenda kule grupuni, ukahamasishe watu watoe michango kwa ajili ya harusi yangu".*
Hapohapo nikakumbuka mtu huyu amekuwepo kwa hilo kundi tangu mwaka 2014, hajawahi kushiriki mambo ya watu yenye uhitaji wa fedha wala muda wake. Tumepitisha mikeka ya kuchangia harusi/send offs za wengine hakuwahi tokea. Tumepitisha mikeka ya kuchangia rambirambi za waliofiwa na waume/wake/wazazi akiwa humo humo hakuna mkeka uliwahi kuonesha jina lake hata kwa kutoa buku tu (1000/=). Muda natafakari naanzaje kuhamasisha watu wajitoe kwa mtu ambaye aligeuza kisogo kwenye mambo ya watu, ndani mwangu nikasikia kitu hicho *_roho ya choyo_*.
_mwlproo_
Roho ya choyo inamfanya mtu kuangalia mambo yake tu. Roho ya choyo inamfanya mtu atamani kukusanya na kujijazia na hata akiwa navyo vingi anabaki mnyimi hatoi kabisa, anaweza kuwa radhi hata kudhulumu (Ezekiel 22:12). Hebu soma haya maandiko hapa chini
*“Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”*
— Wafilipi 2:4
*“Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.”*
— Mithali 21:26
*“Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe;........wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.”*
— Isaya 56:11
Waamini lazima wajifunze kutenda kinyume na roho ya choyo, ndio namna bora ya kuishinda roho hii. Epuka uchoyo, epuka kuwa na umimi, kujiangalia mwenyewe, kujitanguliza mwenyewe. Unatakaje kuvuna kwa watu ambao hukupanda chochote? (Galatia 6:7), unaweza kusema huna hela, lakini hatupandi hela pekee. Panda muda wako kwa wengine, panda vitu, panda ukarimu, jitoe na jihusishe kwenye mambo ya watu. Hakuna kiwango cha kiroho kinachofanya usiweze kuhudhuria harusi za watu, misiba au kuwaona watu wakiwa mahospitalini, hata kwenda kuwaombea basi. Kuna mtu hela zake hakuna mtu anagusa, kuwabariki watu wenye uhitaji hata kwa chakula siku moja tu. Ni mara ngapi unakutana na vitu vizuri mtandaoni iwe ni masomo ya neno la Mungu, nyimbo za Kikristo, au vitu vingine, ukakumbuka hata ku-Copy na ku-Share? inakuwaje vinavyobariki uvienjoi peke yako tu...!!?? Natumia tone ya maisha ya kisasa, kuna wale ambao wao kutwa-kuchwa wanatumia watu links za channels, pages na accounts zao za mtandaoni, wakihamasisha USISAHAU KU-LIKE, KU-SHARE, KU-SUBSCRIBE, NA KUWEKA NOTIFICATIONS ON 🔔, swali mwenzetu ume-Like 👍 za wenzako? ni roho ya choyo tu hapo. Unatuma links kibao kwenye whatsapp groups za watu, ila zikitumwa za kwao kwako unawa-remove dakika 0 tu, sio kawaida ni roho ya choyo tu hapo. Ni roho ya choyo inayokuelekeza nguo zilizokubana uzichome moto badala ya kuwakarimu wengine ambao zingewafaa. Ukiombwa michango ya harusi sijui send off unaweza kushindwa kutoa kiwango chote lakini usiuchune mazima.. tuma hata ka-elfu 5 tu, kuwa umekamatika na kusongwa kwa mengi... Haya ya kuhisi hutahitaji watu kwako yatakutokea puani.. Mambo ya kijamii yanahitaji jamii. Kuna wakati nilishuhudia kwenye mazishi ya ndugu yangu fulani, waliofuata mwili mortuary ni watu baki tu wa mtaani kwa marehemu, walioenda kuchimba shimo bila kudai hata 100/= tshs ni vijana tu wa bodaboda ambao marehemu aliishi akiwaheshimu na kuwasalimia kila akipita... Unapopanda kwa watu (Luka 6:38), unavuna toka kwa watu, na kama ukarimu wako ukiwa mwingi Mungu anaweza sukuma mioyo ya watu wakutegemeze na kukukirimu wewe wakati wa uhitaji (1Samwel 10:26).
Haihitajiki maombi mengi sana, ila kubadili nia/ufahamu kwa kufanya upya na kuanza kutenda kinyume na choyo. Vitu vya thamani kwako, vinavyokupendeza, unavyohisi kuvihitaji zaidi, unavyohisi vinakutosha wewe peke yako.... 👉 Wape watu, wabariki wengine.... vitoe kanisani vikatumike nyumbani mwa Bwana, anza kujifunza kubadili matumizi yako ya luxury kwa kugharimia mahitaji ya lazima ya watu wanaokuhusu na wasiokuhusu. Na yale mambo yanayohitaji uwepo (physical presence) usitume wawakilishi au kutuma hela, kila inapowezekana nenda wewe mwenyewe... Kwa kutenda kinyume na choyo unainyamazisha roho ya choyo
Mungu awabariki sana
0762879363/0765713112
http://alltruthjohn1613.blogspot.co.ke/2016/?m=1
amen ahsante kwa somo zuri
ReplyDelete