Tuesday, November 15, 2022

SWALI NA JIBU (KANUNI YA KUTAFSIRI MAANDIKO)

*KULITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI*

_*Majibu ya swali nililoulizwa na mchungaji mmoja kwa inbox, kufuatia sehemu ya tano ya somo letu*_

Kufuatia sehemu ya tano ya mfululizo wa somo letu la *Kulitumia Kwa Halali Neno La Kweli*, sehemu iliyojikita kuzungumzia *UTOAJI/MATOLEO* nimeulizwa na mchungaji mmoja kuwa Je! kwa namna hiyo niliyofundisha mapato hayatapungua na kurudisha kazi ya Mungu nyuma?

Niseme hivi, watu wanachofanya sasa hivi ni matokeo ya mafundisho, utoaji uliopo sasa hivi (wa kichoyo) ni matokeo ya mafundisho (tena yenye makosa). Kwa fundisho sahihi la Ukristo juu ya utoaji lililojikita juu ya ukarimu (generosity), kanisa wala wahudumu wa injili hawakupaswa kubakia na mahitaji (Mdo 4:34, 2Kor 11:9,  Mdo 20:34-35, Filipi 4:16). Tatizo tulichagua mafundisho yaliyoumodoa Ukristo na watu wakaamini katika Ukristo, utoaji kiwango chake ni kuweka ka-kakapu (kitunga ) na kupokea masilesile 🪙🪙💰💰, au Ukristo kiwango chake ni kutoa million 10 kila upatapo million 100. Ukristo kiwango chake cha utoaji ni kuhudumia mahitaji kwa ukarimu hata pasiwepo uhitaji. Ukipata million 100 kama kuna uhitaji wa million 85, unapambana kuondoa huo uhitaji kwa kadri cha kiasi cha ukarimu wako. Tutawatambua wakristo waliokomaa katika fundisho la Kristo kwa namna yao wanavyohudumia mahitaji ya kazi za injili, na namna wanavyosapoti wahudumu wa injili, ili kusiwe na mikwamo yoyote. Kama waamini wakifundishwa usahihi wa utoaji kiKristo wataacha uchoyo wa kutoa kidogo kwa asilimia wakati uhitaji ni mkubwa. Wakristo wakifundishwa fundisho sahihi la utoaji, mtaona ghafula tu mabadiliko, watu wataanza kutoa magari, hati za nyumba zitamiminika, viwanja vitamiminika, wafanyabiashara wakubwa na watu wenye tenda za mabilioni ya pesa wataacha uchoyo wa percents na badala yake vyombo vya matoleo vitajaa cheques (cheki) za benki zenye figures tu kubwa, mtu hataona kazi kuandika cheki yenye million 700 kuituma kanisani. Ila kwa sasa kwa kuwa mnafundishana uchoyo, mtu anaishi chini ya viwango vya ukristo huku akiamini amefika. Kwa wahudumu wa neno (mafundisho) wafundisheni waKristo mwenendo unaopatana na tabia mpya za asili yao mpya waliyoipata kwa kuzaliwa kwa njia ya Roho wa Yesu. Mapato ya kanisa hayatapungua, badala yake hakutakuwa na mahitaji tena, na itawapunguzia wahubiri kuwa na mahubiri ya mchongo ya *naona watu 50 wenye elfu 50 kwenye wallets 👛  zao, wazitoe na watapata upenyo ndani ya siku 50* 😀 Na wengine wametumia 1Samwel 9:7-9, kuweka gharama za kumwona mtumishi (consultation charges), mara ambatanisha sijui what. All sorts of kuambatanisha, kujiambatanisha kwa sadaka, kuifanya kama catalyst ichochee mchakato wa wewe kupokea ahadi au wema wa Mungu, katika Ukristo vyote hivyo ni vya mchongo. Usiulize swali juu ya haya majibu kama hujasoma sehemu ya 1, 2, 3, 4, 5 ya mfululizo huu. Ukiyakataa haya yakatae tu. Endelea kuufurahia uongo kwamba ikitokea sijui kama hujafanya jambo fulani la kimatoleo utalaaniwa, kwamba utakufa kama Anania na Safira, kwamba hutauona ufalme wa Mungu, kwamba sijui what you name them..... Hayo mmeyachagua kuyaamini kinyume na fundisho la Kristo, mitume wake na matendo yao.......

Asante! Tukutane sehemu ya 6 ambayo iko njiani

Mwl Proo- +255762879363

KANUNI YA KUTAFSIRI MAANDIKO (PART 6)

*KULITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI*
*_Rightly Dividing The Word Of Truth_* (2Timothy 2:15b)

*SEHEMU YA SITA*

_MwlProo-0762879363_

*KUHUBIRI NA KUFUNDISHA (Mathayo 11:1)*
 
Karibu katika mfululizo huu wa kuifahamu kweli, jitahidi usome sehemu tano zilizotangulia utaelewa zaidi hapa. Leo napiga hatua kuingia ndani zaidi. Kuna kipindi fulani hivi katika kanisa, mafundisho mengi yalijengwa juu ya shuhuda za watu waliodai kuchukuliwa mbinguni na kuzimu ma kurudishwa. Wengi wa waliotoa madai hayo hawachukuliwa na shetani, wengi katika wale encounters zao zilikuwa za kweli. Kukatokea tatizo kwa kutojua msingi kamili wa fundisho la Kristo, na hawakuwa na namna sahihi ya kuyafikisha waliyoyaona. Kwa ufinyu wa maarifa ya imani ya Ukristo waliyatafsiri mambo kinyume na kweli, ikapelekea kuwa na vitu vingi kwenye mafundisho vyenye kuwakosesha target waamini. Nyakati hizo mtu angezuka kusema nimemwona mchungaji fulani kuzimu (aliyefariki kitambo) anateseka katika moto, kosa lake alizini kwa siri. Nimemwona bibi yangu kuzimu, kosa lake alikuwa mchawi. Yesu amenionesha kwenye maono wote wanaovaa hereni, mawigi na mikufu wapo motoni wanachomwa, Yesu amenionesha wasiotoa zaka kamili hawana nyumba zao mbinguni, na wanaotoa sadaka chache nyumba zao hazijafungwa lenta au hazina canopy. Kwa hiyo waamini wakawa wakirushwa huku na huko na kila upepo wa fundisho toka katika chanzo kisicho sahihi cha mafundisho na mahubiri. Sipo kinyume na shuhuda zao, nipo kinyume na uwasilisho na tafsiri zinazokinzana na kweli ya injili, pamoja na kutumia maono na ndoto za mbinguni na kuzimu kama chanzo cha mafundisho ya msingi ya kanisa. 

Kwa nini kumetokea makosa (errors) mengi kwenye mafundisho na mahubiri mengi kwenye mwili wa Kristo? Andiko nililoliweka hapo juu (Mathayo 11:1) tunaona wanafunzi wakitumwa kufundisha na kuhubiri. Kuna watu wamepewa karama ya kufundisha, na kuna watu kuhubiri, na inawezekana vyote vikawepo. Mtu ambaye hajapewa kufundisha anapolazimisha kufundisha ni rahisi sana kuwaingiza watu katika makosa. Kuna watu walijaliwa neema ya karama za Roho za matendo ya miujiza, karama za kuponya, na karama zingine zenye mvuto tu, wakaaminika kwamba kama wanaweza kutumika kwa karama za nguvu kiasi hicho wanaweza kufundisha, kwa bahati mbaya ikawa kinyume chake. Miongoni mwa ambao waliingiza chachu nyingi za kimafundisho ni watu waliowahi kutembea katika karama za nguvu _(Rejea somo langu la Karama za Roho)_ na wakaamini pia wanaweza kufundisha, kumbe hawakupewa kufanya hilo (Unaweza ukaelewa fundisho la mtu aliyetoka kufufua mfu, linavyoweza kuwa na nguvu, hata kama lina makosa. Watu waliondaliwa na kupewa huduma ya kufundisha wanayo neema ya kufanya uchambuzi wa maandiko (exposition of  scriptures) na kuleta *BALANCE* ya mambo yote yahusuyo imani. Nimesoma kisa fulani ambapo Kenneth Hagin alimwandikia mwalimu mmoja wa neno la Mungu kwa jina Gordon Lindsay (ambaye aliwahi kuwa manager wa mhubiri wa miujiza na uponyaji aitwaye William Branham), katika ujumbe wake alimwambia nimeona maono kadhaa moja wapo ilikuwa Bwana anamwondoa Branham kwa sababu ya damage anayoileta kwenye mwili wa Kristo kimafundisho. Baada ya miezi kadhaa kupita na mhubiri huyo kupatikana katika ajali ya gari na kuwa katika comma na badae kufariki, Lindsay alimjibu Hagin kuwa mtu uliyetoa unabii juu yake amefariki. Lindsay alisisitiza kusema, nilimwambia brother Branham wewe si mwalimu, unachanganya waamini, hubiri neno kisha tumia karama za miujiza na kuponya. Majibu ya Branham kwa Lindsay yalikuwa, "najua mimi si mwalimu, lakini nataka kufundisha, na nitafundisha". Unaweza kuwa na karama kuu za kiroho zenye mvuto mwingi, ila kama hukupewa kufundisha kila ufanyapo hivyo unaweza kuwaelekeza watu katika makosa. Kabla ya Lindsay kuondoka kwenye utumishi wa Branham alisaidia kuleta balance ya mambo mengi kimafundisho (NB:- SIPO KINYUME NA HAWA WOTE NILIOWATAJA AKIWEMO HUYO BRANHAM W.M, NIMETUMIA KISA CHAO KUFUNDISHA TU).

Siku moja nikiwa naandika ufafanuzi wa sura 12 za Daniel (April 2020), nilipofika sura ya 7, 8, 9, & 12 nikajigundua nimekaa nikiwa natumia nyenzo kadhaa mpaka scientific calculator (Niliandika masomo hayo baada ya Mungu kwa Roho Mtakatifu kuniahidi katika ndoto kuwa wiki hiyo atanipa kuelewa hicho kitabu). Nikasema Mungu kama imenibidi nipitie haya ili kukielewa kitabu hiki  Je! itakuwaje kwa wengine ambao labda hawana kipawa cha hivyo, ilikusudiwa wote waelewe? hapo hapo jibu la Mungu kwangu likawa, kila mahali kuna watu waliopewa vipawa vya kufanya uchambuzi wa maandiko (Labda kama hawatatumiwa, au kunyamazishwa). Na hapa niandike ushauri tu kwa viongozi wa makanisa, wasizime vipawa vya waliopewa kufundisha, kwa kuwa unaweza kuwa senior pastor lakini labda una neema ya kuhubiri tu si kufundisha, ukawa na watu dhaifu kwa upande wa fundisho la Kristo, wakasombwa na ukengeufu wowote utakaojitokeza, kumbe hawakupata nafasi ya kufundishwa. Nimesoma andiko la mtu mmoja kasema walimu wanaofundisha masomo ya neema wanapenda sana kutumia maneno ya kiyunani na kiebrania na wanatumia ufahamu wao zaidi kuliko ufunuo wa Roho. Walimu wanaweza kuwa na neema tofauti ya kufanya uchambuzi (exposition of scriptural text), ukiwaona huko kwako *WATUMIE*, USIWAPINGE, USISIMAME NAO KINYUME. Kama unakerwa na ufafanuzi wa kutumia Kiyunani na Kiebrania ni wazi tu, hukupewa eneo hilo kutumika na approach hiyo, shughulika na mzingo na mlinganyo uliopewa utumike kwa uaminifu, lakini waliopewa kipawa cha kufundisha wapewe nafasi hiyo ili kuleta balance ya kweli yote ya injili. Ilitolewa kazi kwa wanafunzi *Wafundishe na kuhubiri*,  watu hawawezi kujengwa kwa ukamilifu kwa kuhubiriwa peke yake, kuna mahali fulani hawatafika kimaarifa ya kiroho. Waamini waliojengwa katika kuhubiriwa pekee bila kufundishwa hawawi imara kiasi cha kusimama sana wao wenyewe. Hawa ndio ambao wakipata uhamisho wa kikazi mbali na mahubiri aliyozoeaga kumpiga *handel*, hasongi mbele, hawa ndio ambao mtumishi anayewaongoza kiroho akifariki na wao hawaendelei tena mbio zao za imani, hawa ndio kukitokeza kauvumi ka roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani yanawabeba alfajiri na mapema.

Kama nilivyotangulia kusema, imani ya Ukristo sio ya mchongo. Mafundisho yasiyojengwa au kutokana na kweli ya injili  lazima yawe *terminated*, mafundisho ambayo msingi wake ulikuwa ndoto na maono binafsi ya mtu huku yakikinzana na fundisho la Kristo, na mitume wake na matendo yao sharti liondolewe lisiweke kwazo wala kongwa la utumwa kwa waamini. Waliopewa kuhubiri wahubiri tu, wasijaribiwe kufundisha waka-infuse errors kwa mafundisho yenye makosa (false indoctrination). Waliopewa kufundisha, wafundishe kwa bidii, kwa ustahimilivu, wala wasichoke. Mwili wa Kristo (kanisa) ujazwe kwa maarifa sahihi ya neno la Mungu, na kuwasaidia waamini kuweza kusimama nyakati zote, na kuwa wazoevu wa maneno ya imani. Hawa wataweza kushinda purukushani zote za masuala ya kiimani katika dunia hii mbovu.


Mungu awabariki tukutane sehemu ya 7

alltruth5ministries@gmail.com

Wednesday, November 2, 2022

KANUNI YA KUTAFSIRI MAANDIKO (PART 5)

*KULITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI*
_*Rightly Dividing The Word of Truth*_ (2Timothy 2:15b)
*_Na Mwl Proo_*

*SEHEMU YA TANO* 

```MATOLEO/UTOAJI```

Ili kuepuka kuuliza maswali ambayo yamekwishajibiwa na mfululizo huu, tafadhali soma sehemu nne zilizotangulia. 
Mpaka hapa tulipofika tumeanza kuelewa kuhusu imani yetu ya kumfuata Kristo (Ukristo), tumejua kwa sehemu kubwa kuhusu mwenendo wa waamini, tumeanza pia kufahamu matumizi halali ya neno la kweli. Katika sehemu zilizotangulia tuliona kuwa imani ya kumfuata Kristo (Ukristo) sio imani ya kuunga-unga, haijakosa fundisho la msingi, haihitajiki kujiongeza (mafundisho ya mchongo) kana kwamba kweli haipo. Leo nitazungumzia suala moja tu la muhimu sana yaani UTOAJI (MATOLEO) kwa sura ya Ukristo. 

Nianze kwa kusema, *_"KAMA KUNA FUNDISHO LOLOTE LITAKALOKUELEKEZA WEWE MWAMINI UACHE KUWA MTOAJI, NI LA KULIKATAA, KWA SABABU UKARIMU NI TABIA YAKO KIASILI KWA ASILI MPYA ULIYOIPATA KWA KUWA NDANI YA KRISTO, KIUMBE KIPYA_* 

Pamoja na ukweli huo, bado unahitajika kujifunza usahihi wa utoaji. Hapa inahitajika uvue miwani 👓 ya kidini na kidhehebu, uweze kuufahamu usahihi wa maandiko na mafundisho kwenye imani hii. Haya ninayofundisha sasa si lazima sana yapatane na kile ulichowahi kufundishwa... Haya yanapatana na ile kweli ya injili, hicho ndicho nina hakika nacho 100%.

Mimi Mwl Proo ni mthiolojia kitaaluma, nilipata kujifunza _Jewish Korbanot Systems_ yaani mifumo ya matoleo ya kiyahudi. Matoleo ya sadaka ya dhambi, ya amani, za kuteketeza, za vyakula zote kwa aina zake na mitindo yake... mafuta, unga, ndege, wanyama na chochote vilikuwa ni mifano (typology) ya sadaka moja ya badae ambayo ilitolewa toka mwanzo. Bila ku-panic soma kwa utulivu tena (Waebrania 10:1-10). 

Jamii ya waamini, baada ya kufa na kufufuka kwa Kristo haiwi tena na mwenendo ule wa kivuli (Kol 2:17, Ebr 10:1), haiongozwi na kiongozi (Gal 3:24, Rumi 10:4) ambacho kiliwekwa kutuleta kwa Kristo tu.

Kutoka katika ufahamu huu, huwezi nyofoa kamstari katika Walawi, bila hata ufahamu wa kutosha wa matoleo ya kiyahudi, ukawaambia waamini jamani neno limesema sadaka ya kuinuliwa, sijui ya kutikiswa, hapana!. 

Leo hii kuna mafundisho mengi ya ovyo-ovyo kama sio ya kujichanganya na ya kinafiki (rough, hypocritic & confusing teachings) kuhusu utoaji, ni kwa vile kulikosekana nafasi ya fundisho la msingi la kanisa pahala pengi, hiyo ikapelekea matumizi yasiyo halali ya neno la kweli. Mafundisho mengi yana mzani wa hadaa (Double-Standard), yaani mtu anataka kwa wakati mmoja atumike na huduma ya mauti, wakati mchache badae atumike na huduma ya roho na ya haki (2Kor 3:7-11).

Leo ninawashangaza kidogo, kuwa mfumo wote wa utoaji, aina zote za matoleo, ikiwa ni pamoja na nia ya kutoa kama ilivyoelezwa kama picha kwenye Torah (Sheria ya Musa) hazihusiki kabisa kwenye imani ya Ukristo (THEY ARE ALL IRRELEVANT IN CHRISTIANITY). Sijachanganyikiwa, wala sijakopi fundisho la watu wala taasisi yoyote. Hiki ndicho kilichopo kwenye imani ya Ukristo, na nitakuonesheni.

 Ndugu zangu waKristo, katika utekelezaji wa sheria 613 (Decalogue inclusive) za Musa kama ulivyofafanuliwa vyema katika Talmud ya wayahudi, ni kosa kubwa kutimiza sheria 599 kwa ukamilifu ukaiacha moja ya 600 (Yakobo 2:10). Ni mchezo wa kuigiza (hypocrisy) katika ulimwengu wa torati kusema unatoa malimbuko (Walawi 23:10), halafu hautoi kodi ya Bwana (Hesabu 31:37, 38, 39). Kwa wasiojua Torati ya Musa, mbali na zaka ambayo kimsingi ni 23%, wayahudi waliamriwa pia kulipa *Kodi ya Bwana* ambayo ni 0.2%, ukitoa zaka ya fungu la kumi (Kumb 22:14), halafu ukaacha kulipa kodi ya Bwana ambayo ni 0.2% wewe ni mnafiki, mwigizaji, mvunja sheria yote, ustahiliye kupata hukumu (Jiulizeni huko kwenu, lini mlitoa kodi ya Bwana? jibu liwajuze kuwa mnaenenda kwa unafiki au kwa ujinga).

Kanisa la mitume (early church) waliweza kutofautisha utoaji kwa waamini, na utoaji waliouzoea mwanzoni wa kiyahudi (kama ilivyoamuru torati). Hawakuendelea na desturi zozote za utoaji za kiyahudi kwenye Ukristo. Kwa nini hawakuendelea nazo, hazikuwa relevant. Fanya study yoyote utakayoiweza ya kanisa lile la mwanzo, hutakutana na utoaji wowote kutoka katika _jewish korbanot system_. Ni wanafunzi wasio makini (careless learners) wa maandiko ndio wanaruka-ruka na mistari nje ya muktadha, utasikia Mathayo 23:23 na Luka 11:42, Yesu amesema wala msiache yale mengine 😂😂😂. The Bible Is The Book Of Context (Biblia ni kitabu cha muktadha), hao Mafarisayo (wa chini ya sheria) na Yesu mwenyewe amezaliwa chini ya sheria, walipaswa kuzingatia yote yaliyowahusu chini ya sheria.. iwe tohara, iwe sadaka za kuteketeza na vyakula n.k. Huwezi kurupuka na huo mstari uwasomee waamini kanisani, huku ukiwahimiza jamani Yesu alisema msiache yale mengine.. Huo ni udanganyifu, na matumizi yasiyo halali ya neno la kweli. Kaa chini ujifunze, Je! mitume wa Yesu, kanisa la awali, waliendelea na desturi za matoleo ya kiyahudi? Je! wakristo wa mwanzo huko Uyunani, Uturuki etc walipokutana kwenye makusanyiko yao (kwenye nyumba za watu) hata kabla hawajajenga majengo ya kuabudia, Je! walitoa matoleo ya kiyahudi yoyote? JIBU KUTOKA KATIKA HIYO STUDY YAKO NI *HAPANA*

Ni hivi, wale wa tohara, wale waliopewa sheria walipojaribu kuifuata sana sheria ili kuitenda, walionekana kumpendeza Mungu. Ila waKristo kila wajaribupo kuyafuata maelekezo ya sheria ya Musa kama namna na ya kumcha Mungu, wanamhuzunisha kwa huo ujinga. Najua kiu yenu kubwa sasa, ni Je! tutoeje sasa..!!!! Unasoma kitu sahihi sasa. Katika Ukristo kuna  aina mbili tu za matoleo, ambazo naweza kuzifundisha kwa Biblia, naweza andika vitabu vingi, naweza kueleza na kuthibitisha kwa ushahidi mwingi. Aina hizo za matoleo (utoaji), ni 

1. Sadaka za hiari. Watu kuamua wao wenyewe kwa ukarimu wao watoe nini kwa kiasi gani. Hapa hawapangiwi watoe ngapi, hawatishiwi wasipotoa kupatikana na mabaya yoyote...  (2Korintho 9:7)

2. Changizo (michango) 👉 1Korintho 16:1, Waroma 15:26

Sadaka za hiari (kutokana na ukarimu na tabia ya upendo), na changizo ndiyo matoleo yanayohusiana na imani ya Ukristo... mnaweza kuzipa majina mengi lakini kunabakia makundi hayo mawili. Wakristo hawapaswi kutoa kichoyo kama wale wa jangwani wenye mioyo migumu waliopewa torati. Wakristo wanatoa kwa kadri ya uhitaji, hata pasiwepo upungufu. Kama una million 200 na uhitaji ni million 180, utatoa million 180 kuondoa uhitaji uliopo na sio million 20, kuacha watu wapambane na uhitaji wa million 160. Katika ukristo kama kunahitajika ada za watoto wa mchungaji na jumla ya ada ni million 7, badala ya kuweka kaubunifu ka kitapeli (fraudulence)... kwamba nitagawa bahasha za kinabii (prophetic envelopes) ✉️✉️✉️✉️✉️ weka sadaka inayouma, uuguse moyo wa Mungu.... wekeni tu changizo kupata hizo million 7 basi. Matoleo katika Ukristo ni sadaka ambazo watu watatoa wenyewe kwa kuamua wao viwango, na nje hapo ni changizo (michango)..... *CHOCHOTE NJE YA HAPA NI CHA MCHONGO, SADAKA YOYOTE ILIYOAMRIWA NA MUSA IKILETWA KANISANI NI YA MCHONGO, HAINA UHUSIANO NA UKRISTO.* Usikasirike huu ni ukweli, hata kama baada ya hapa tutaendelea na desturi  za dini na madhehebu yetu, tuendelee na mazoea yetu tukiwa tumeshaufahamu ukweli na usahihi.
_mwlproo_
Kuna watu kadhaa wamejirudi wenyewe siku za usoni, huku wakisema katika Agano Jipya (ambalo nalo hawalijui wanahisi ni hivi vitabu/barua 27) kwamba tunatoa malimbuko na zaka kwa upendo sio kwa mujibu wa sheria. Kwa wakati huo huo bado wananukuu Malaki 3:8-11. Ili Malaki 3:8-11 iwe katika kutumika (in effect) ni lazima Malaki 4:4 iwe katika kutumika... Sheria na amri haziwekwi bila hukumu zake.... Yaani ukimriwa usizini, basi kuna hukumu yake ukiivunja upigwe mawe. Double Standards nilizozitaja mwanzo ni kuchagua kaupande kamoja, na kukatupa nje kaupande kengine (unafiki/ujinga 👉 one of the two is correct).
Mara kadhaa nasikia watu wakiombea sadaka wananukuu Kutoka 34:20b, kwamba Mungu ulisema tusije mbele zako mikono mitupu. Nyie watu!!!!!!!  mnadhani kila agizo la torati mliambiwa ninyi? Kwa taarifa yenu Wakristo hawatoi matoleo kwamba wameagizwa, HAPANA! Tabia ya ukarimu (generosity) ya Baba yao (Mungu) ipo ndani yao tayari kwa kuzaliwa kwa pili... Kutoka katika huo ukarimu ndio wanatoa.. Kama hawatoi haina maana hawajazaliwa na Mungu, wafundishwe tu mafundisho sahihi ya injili, watambue asili yao mpya ina tabia zipi, watatoa mpaka hakutakuwa na uhitaji. Kuamini kwamba Mungu amewaagiza msiende mbele zake bila kitu mkononi ni kujifunga kwenye kongwa la utumwa.... PIA KILA ITAKAPOTOKEA UMEHUDHURIA IBADA UKIWA HUNA SADAKA, ITAHESABIWA KUWA NI DHAMBI. Wakristo wakomavu hawawezi kuwa kwenye makusanyiko ya ibada bila fedha na mali za kusapoti kazi ya Mungu, na kusapoti maisha ya wanaoitenda kazi ya Mungu. Lakini si kwa agizo la KUTOKA 34:20b, na hivyo kama hawana wasiache kuhudhuria, na wasipotoa hawakuhumiwi wala kulaaniwa. Yale mengine ya mchongo mfano:-kuhimizana kuwa ukiweka nadhiri (vowed offerings) inamhamasisha Mungu atende kwa haraka, ni maudambudambu tu ya kidini nje ya muktadha wa Kikristo. Baba yake Yesu ambaye ni Baba yetu hahitaji kupigwa _Handel_ ili kumhamasisha awe mwema au mkarimu. Hasubiri ahadi za 'ee Mungu nikipata ile kazi, nitanunua viti vya kanisani....' Yeye kwa njia Yesu, pamoja na Yesu amekupa vyote, unaweza kupata chochote (Waroma 8:32). Ila kama mnapenda kuwa na vitu vya mchongo endeleeni kuweka nadhiri mkiamini Yesu na mitume wake walipitiwa kuwafundisha tabia za Baba yenu wa Mbinguni!

*KUHUSU LAANA* 
Wakristo wapuuziaji (Careless Christians) ndio  pekee wanasoma Malaki 3:9 na kuamua kulibinafsisha hili andiko.... Kuwa nimelaaniwa kwa laana, na taifa hili lote.... kisa nini?????? Eti nilipewa elfu 2 ya nauli na sikuitolea 10% yaani  shilingi 200. So unahisi Yesu na Baba Yake (Mungu) wanashirikiana kukulaani kila wakigundua kuna msimbazi ulipewa 10,000/= na hukutoa buku (1000/=) bali uliitumia yote kulipa deni fulani pale  Mangi Shop????😝😝😝😝
_mwlproo_
Ndugu zangu katika Kristo, hakuna laana inayokuja kwa mtoto wa Mungu toka kwa Baba yake kisa amekosea au kutofanya jambo fulani bila ukamilifu. Si tabia ya Mungu, na wala shetani hawezi. Na huo ndio mvuto wa kuiamini injili. Hakuna mtu anayeweza kukulaani wewe mwamini, mwenye maarifa sahihi ya Yesu. Tena kama kuna kiongozi wa kiroho aliwahi kukulaani na ukalaanika, hii inawezekana tu kwa kuwa wewe umejiweka (submit)  chini yake kifundisho na maongozi ya kiroho.. Ambako hapo napo bado itategemea una-operate kwa kiwango kipi katika maarifa ya kiroho (ya kumfahamu sana Mwana wa Mungu, Yesu Kristo)... Otherwise mikwamo yote unayokutana nayo, sio matokeo ya kulaaniwa...USIIBIWE, unaweza kutoka tu kuyatumia mamlaka yako uliyoyapewa na Kristo na kufanya bidii ya kazi na matendo mema... 

*UKIRI*
Mimi ni mwamini, nimebarikiwa. Nitafanya kazi kwa bidii, nipate fedha na mali za kusaidia uhitaji na wahitaji. Nitatoa daima maana ndio tabia yangu katika Kristo. Bwana wangu Yesu amenionesha njia njema, kuwa ni bora kutoa kuliko kupokea (Matendo 20:35). Hivyo nitatoa, kama Bwana wangu alivyo mkarimu, mimi pia nitaonesha ukarimu kwa kutoa sana sana sana.


USIKOSE SEHEMU YA SITA (6) YA SOMO HILI TUTAPIGA HATUA KUINGIA NDANI ZAIDI

0762879363 (WhatsApp)

alltruth5ministries@gmail.com